1:1 Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene,
1:2 tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Ninyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia.
1:3 Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
1:4 Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia ninyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu.
1:5 Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri,
1:6 kwani, ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu,
1:7 hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
1:8 Yeye atawaimarisha ninyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia Siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.
1:9 Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita ninyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.
1:10 Ndugu, ninawasihi kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja.
1:11 Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonyesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu.
1:12 Nataka kusema hivi: kila mmoja anasema chake: mmoja husema, "Mimi ni wa Paulo," mwingine: "Mimi ni wa Apolo," mwingine: "Mimi ni wa Kefa," na mwingine: "Mimi ni wa Kristo,".
1:13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?
1:14 Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo.
1:15 Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu.
1:16 (Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.)
1:17 Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe.
1:18 Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu ujumbe huo ni nguvu ya Mungu.
1:19 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali."
1:20 Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa Sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu.
1:21 Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri.
1:22 Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima;
1:23 lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu;
1:24 lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu.
1:25 Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara zaidi kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu zaidi kuliko nguvu za binadamu.
1:26 Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka ya juu.
1:27 Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu.
1:28 Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana.
1:29 Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu.
1:30 Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha ninyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa.
1:31 Basi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mwenye kutaka kujivuna, basi, na ajivunie kazi ya Bwana."
2:1 Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu.
2:2 Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa.
2:3 Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi.
2:4 Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho.
2:5 Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu.
2:6 Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea.
2:7 Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu.
2:8 Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangalielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu.
2:9 Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao."
2:10 Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu.
2:11 Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.
2:12 Sasa sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu.
2:13 Basi sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho.
2:14 Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho.
2:15 Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine.
2:16 Maandiko yasema: "Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?" Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.
3:1 Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo.
3:2 Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari.
3:3 Maana bado mu watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na magombano kati yenu? Mambo hayo yanaonyesha wazi kwamba ninyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia.
3:4 Mmoja wenu anaposema, "Mimi ni wa Paulo", na mwingine, "Mimi ni wa Apolo", je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu?
3:5 Apolo ni nani? na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni ninyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana.
3:6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu.
3:7 Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota.
3:8 Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe.
3:9 Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na ninyi ni shamba lake; ninyi ni jengo lake.
3:10 Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake.
3:11 Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo.
3:12 Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi.
3:13 Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati Siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, Siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonyesha ubora wake.
3:14 Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo;
3:15 lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
3:16 Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
3:17 Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni ninyi wenyewe.
3:18 Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli.
3:19 Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: "Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao."
3:20 Na tena: "Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai."
3:21 Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu.
3:22 Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu.
3:23 Lakini ninyi ni wa Kristo naye Kristo ni wa Mungu.
4:1 Mtu na atuone sisi kuwa ni watumishi wa Kristo tuliokabidhiwa siri za mungu.
4:2 Kinachotakiwa kwa yeyote yule aliyekabidhiwa kazi ni kuwa mwaminifu.
4:3 Kwangu mimi si kitu nikihukumiwa na ninyi, au na mahakama ya kibinadamu; wala sijihukumu.
4:4 Dhamiri yangu hainishtaki kwa jambo lolote, lakini hiyo haionyeshi kwamba sina lawama. Bwana ndiye anayenihukumu.
4:5 Basi, msihukumu kabla ya wakati wake acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yaliyofichika, na kuonyesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.
4:6 Ndugu, hayo yote niliyosema juu ya Apolo na juu yangu, ni kielelezo kwenu: kutokana na mfano wangu mimi na Apolo nataka mwelewe maana ya msemo huu: "Zingatieni yaliyoandikwa." Kati yenu pasiwe na mtu yeyote anayejivunia mtu mmoja na kumdharau mwingine.
4:7 Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa?
4:8 Haya, mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tuweze kutawala pamoja nanyi.
4:9 Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu.
4:10 Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, ninyi ni wenye nguvu. Ninyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa.
4:11 Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi.
4:12 Tena twataabika na kufanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa, tunawatakia baraka; tukidhulumiwa, tunavumilia;
4:13 tukisingiziwa, tunajibu kwa adabu. Mpaka sasa tumetendewa kama uchafu wa dunia; na kwa kila mtu sisi ni takataka!
4:14 Siandiki mambo haya kwa ajili ya kuwaaibisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwafundisheni watoto wangu wapenzi.
4:15 Maana hata kama mnao maelfu ya walezi katika maisha yenu ya Kikristo, baba yenu ni mmoja tu, kwani katika maisha ya Kikristo mimi ndiye niliyewazaeni kwa kuihubiri Habari Njema.
4:16 Kwa hiyo, nawasihi: fuateni mfano wangu.
4:17 Ndiyo maana nimemtuma Timetheo kwenu. Yeye ni mtoto wangu mpenzi na mwaminifu katika Bwana. Atawakumbusheni njia ninayofuata katika kuishi maisha ya Kikristo; njia ninayofundisha kila mahali katika makanisa yote.
4:18 Baadhi yenu wameanza kuwa na majivuno wakidhani kwamba sitakuja tena kwenu.
4:19 Lakini, Bwana akipenda, nitakuja kwenu upesi; na hapo ndipo nitakapojionea mwenyewe, sio tu kile wanachoweza kusema hao wenye majivuno, bali pia kila wanachoweza kufanya.
4:20 Maana Utawala wa Mungu si shauri la maneno matupu, bali ni nguvu.
4:21 Mnapendelea lipi? Nije kwenu na fimbo, ama nije na moyo wa upendo na upole?
5:1 Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake!
5:2 Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu.
5:3 Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu.
5:4 Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu,
5:5 mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana.
5:6 Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga?
5:7 Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko.
5:8 Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli.
5:9 Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi.
5:10 Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa!
5:11 Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye.
5:12 Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe?
5:13 Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!
6:1 Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu?
6:2 Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo?
6:3 Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika?
6:4 Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa?
6:5 Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini?
6:6 Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini.
6:7 Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa! Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyang'anywa mali yenu?
6:8 Lakini, badala yake, ninyi ndio mnaodhulumu na kunyang'anya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu!
6:9 Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti,
6:10 wevi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang'anyi, hao wote hawatashiriki Utawala wa Mungu.
6:11 Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
6:12 Mtu anaweza kusema: "Kwangu mimi kila kitu ni halali." Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote.
6:13 Unaweza kusema: "Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula." Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili.
6:14 Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake.
6:15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo!
6:16 Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye--kama ilivyoandikwa: "Nao wawili watakuwa mwili mmoja."
6:17 Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye.
6:18 Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
6:19 Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi, si mali yenu wenyewe.
6:20 Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
7:1 Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: naam, ni vizuri kama mtu haoi;
7:2 lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.
7:3 Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe.
7:4 Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo.
7:5 Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu.
7:6 Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri.
7:7 Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.
7:8 Basi, wale ambao hawajaoana na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo.
7:9 Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia basi, na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa.
7:10 Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: mke asiachane na mumewe;
7:11 lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe.
7:12 Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka.
7:13 Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe.
7:14 Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu.
7:15 Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni ninyi muishi kwa amani.
7:16 Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo?
7:17 Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote.
7:18 Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe.
7:19 Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu.
7:20 Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
7:21 Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie.
7:22 Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo.
7:23 Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu.
7:24 Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa.
7:25 Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa.
7:26 Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo.
7:27 Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa.
7:28 Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate ninyi.
7:29 Ndugu, nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa;
7:30 wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu;
7:31 nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita.
7:32 Ningependa ninyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana.
7:33 Mtu aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe,
7:34 naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe.
7:35 Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuio. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja.
7:36 Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi.
7:37 Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira.
7:38 Kwa maneno mengine: yule anayeamua kumwoa huyo mchumba wake anafanya vema; naye anayeamua kutomwoa anafanya vema zaidi.
7:39 Mwanamke huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo.
7:40 Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu.
8:1 Yahusu sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi, lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga.
8:2 Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa.
8:3 Lakini anayempenda Mungu huyo anajulikana naye.
8:4 Kwa hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu.
8:5 Hata kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu na mabwana wengi,
8:6 hata hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu: Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake.
8:7 Lakini, si kila mtu anao ujuzi huu. Maana wako watu wengine waliokwisha zoea sanamu, watu ambao mpaka hivi sasa wanapokula vyakula huviona bado kama vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Na kwa vile dhamiri zao ni dhaifu, hutiwa unajisi.
8:8 Lakini chakula hakiwezi kutupeleka karibu zaidi na Mungu. Tukiacha kukila hatupungukiwi kitu, tukikila hatuongezewi kitu.
8:9 Lakini, jihadharini: huu uhuru wenu usiwafanye walio na imani dhaifu waanguke katika dhambi.
8:10 Maana, mtu ambaye dhamiri yake ni dhaifu, akikuona wewe mwenye ujuzi unakula vyakula hivyo ndani ya hekalu la sanamu, je, hatatiwa moyo wa kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu?
8:11 Hivyo, huyo ndugu yako dhaifu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, atapotea kwa sababu ya ujuzi wako.
8:12 Kama mkiwakosesha ndugu zenu jinsi hiyo na kuzijeruhi dhamiri zao dhaifu, mtakuwa mmemkosea Kristo.
8:13 Kwa hiyo, ikiwa chakula husababisha kuanguka kwa ndugu yangu, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi.
9:1 Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, ninyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana?
9:2 Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu ninyi mimi ni mtume. Ninyi ni uthibitisho wa mtume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana.
9:3 Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii:
9:4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa?
9:5 Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa?
9:6 Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi?
9:7 Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake?
9:8 Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, Sheria nayo haisemi hivyo?
9:9 Imeandikwa katika Sheria ya Mose: "Usimfunge kinywa ng'ombe anapoliwata nafaka." Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe?
9:10 Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; kwani yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno.
9:11 Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia?
9:12 Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao? Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo, Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo.
9:13 Je, hamjui kwamba wanaotumikia Hekaluni hupata chakula chao Hekaluni, na kwamba wanaotolea sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka?
9:14 Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo.
9:15 Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure.
9:16 Ikiwa ninaihubiri Habari Njema, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri Habari Njema!
9:17 Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadam naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze.
9:18 Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.
9:19 Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo.
9:20 Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya Sheria, nimejiweka chini ya Sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya Sheria.
9:21 Na kwa wale walio nje ya Sheria, naishi kama wao, nje ya Sheria, ili niwapate hao walio nje ya Sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo.
9:22 Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia.
9:23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Habari Njema, nipate kushiriki baraka zake.
9:24 Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi?
9:25 Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji ya kudumu daima.
9:26 Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani.
9:27 Naupa mwili wangu mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili, nisije mimi mwenyewe nikakataliwa baada ya kuwahubiria wengine.
10:1 Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari.
10:2 Wote walibatizwa katika umoja na Mose kwa lile wingu na ile bahari.
10:3 Wote walikula chakula kilekile cha kiroho,
10:4 wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe.
10:5 Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani.
10:6 Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani.
10:7 Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: "Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza."
10:8 Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu ishirini na tatu elfu.
10:9 Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka.
10:10 Wala msinung'unike kama baadhi yao walivyonung'unika, wakaangamizwa na Mwangamizi!
10:11 Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili.
10:12 Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke.
10:13 Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
10:14 Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu.
10:15 Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo.
10:16 Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo?
10:17 Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.
10:18 Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu.
10:19 Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu?
10:20 Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na ushirika na pepo.
10:21 Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo.
10:22 Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?
10:23 Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga.
10:24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake.
10:25 Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu;
10:26 maana Maandiko yasema: "Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana."
10:27 Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu.
10:28 Lakini mtu akiwaambieni: "Chakula hiki kimetambikiwa sanamu," basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile.
10:29 Nasema, "kwa ajili ya dhamiri," si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: "Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine?
10:30 Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?"
10:31 Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
10:32 Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu.
10:33 Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.
11:1 Niigeni mimi kama ninavyomwiga Kristo.
11:2 Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni.
11:3 Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo.
11:4 Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo.
11:5 Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake.
11:6 Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake.
11:7 Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume.
11:8 Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume.
11:9 Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume.
11:10 Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika.
11:11 Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke.
11:12 Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu.
11:13 Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani?
11:14 Hata maumbile yenyewe huonyesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe;
11:15 lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike.
11:16 Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine.
11:17 Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa ninyi hongera kuhusu haya yafuatayo: mikutano yenu ninyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida.
11:18 Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi,
11:19 maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana.
11:20 Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula chakula cha Bwana!
11:21 Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa!
11:22 Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili.
11:23 Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu aliotolewa, alitwaa mkate,
11:24 akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: "Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka."
11:25 Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe akasema: "Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka."
11:26 Maana kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja.
11:27 Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
11:28 Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho;
11:29 maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.
11:30 Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa.
11:31 Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo.
11:32 Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
11:33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula chakula cha Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake.
11:34 Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.
12:1 Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya:
12:2 Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu.
12:3 Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: "Yesu alaaniwe!" Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: "Yesu ni Bwana," asipoongozwa na Roho Mtakatifu.
12:4 Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja.
12:5 Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja.
12:6 Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.
12:7 Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote.
12:8 Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu apendavyo Roho huyohuyo.
12:9 Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya;
12:10 humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua.
12:11 Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.
12:12 Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote--ingawaje ni vingi--hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo.
12:13 Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.
12:14 Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi.
12:15 Kama mguu ungejisemea: "Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili", je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha!
12:16 Kama sikio lingejisemea: "Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili", je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La!
12:17 Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa?
12:18 Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda.
12:19 Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
12:20 Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja.
12:21 Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: "Sikuhitaji wewe", wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: "Siwahitaji ninyi."
12:22 Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi.
12:23 Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi,
12:24 ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima,
12:25 ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane.
12:26 Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho.
12:27 Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.
12:28 Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni.
12:29 Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza?
12:30 Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha?
12:31 Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote.
13:1 Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele.
13:2 Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu.
13:3 Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote.
13:4 Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni.
13:5 Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya,
13:6 hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli.
13:7 Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.
13:8 Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita.
13:9 Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili.
13:10 Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka.
13:11 Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadam mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha.
13:12 Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi.
13:13 Sasa yanadumu haya matatu: imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.
14:1 Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu.
14:2 Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika.
14:3 Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo.
14:4 Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa.
14:5 Basi, ningependa ninyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa.
14:6 Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani.
14:7 Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa?
14:8 La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita?
14:9 Hali kadhalika na ninyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani.
14:10 Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana.
14:11 Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu.
14:12 Hali kadhalika na ninyi, maadam mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa.
14:13 Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua.
14:14 Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure.
14:15 Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu.
14:16 Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema: "Amina," kama haelewi unachosema?
14:17 Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini huyo mwingine haitamfaidia.
14:18 Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni zaidi kuliko ninyi nyote.
14:19 Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema maneno elfu ya lugha ngeni.
14:20 Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu muwe kama watoto wachanga lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu waliokomaa.
14:21 Imeandikwa katika Sheria: "Bwana asema hivi: Kwa njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza."
14:22 Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili ya wasioamini.
14:23 Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je, hawatasema kwamba ninyi mna wazimu?
14:24 Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu.
14:25 Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na kumwabudu Mungu akisema: "Kweli Mungu yupo pamoja nanyi."
14:26 Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa.
14:27 Wakiwepo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa.
14:28 Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu.
14:29 Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao.
14:30 Ikiwa mmoja anaposema mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze.
14:31 Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo.
14:32 Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji.
14:33 Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani.
14:34 Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema; ila wawe watii kama isemavyo Sheria.
14:35 Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini.
14:36 Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu ninyi au kwamba limewajieni ninyi peke yenu?
14:37 Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia ninyi ni amri ya Bwana.
14:38 Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu huyo.
14:39 Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni.
14:40 Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu.
15:1 Sasa ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake.
15:2 Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure.
15:3 Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu;
15:4 kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa;
15:5 kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili.
15:6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
15:7 Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote.
15:8 Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.
15:9 Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.
15:10 Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo. Na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami.
15:11 Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachuhubiri, na hiki ndicho mnachoamini.
15:12 Sasa, maadam inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu?
15:13 Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka;
15:14 na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana.
15:15 Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu na kumbe yeye hakumfufua--kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi.
15:16 Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka.
15:17 Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu.
15:18 Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa.
15:19 Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani.
15:20 Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, limbuko lao wale waliolala katika kifo.
15:21 Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka wafu kumesababishwa na mtu mmoja.
15:22 Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.
15:23 Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza, halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja.
15:24 Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba Utawala, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu.
15:25 Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake.
15:26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo.
15:27 Maana, Maandiko yasema: "Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake." Lakini, Maandiko yanaposema: "Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale" ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo.
15:28 Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya Utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya Utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote.
15:29 Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao?
15:30 Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa?
15:31 Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili.
15:32 Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, "Tule na tunywe, maana kesho tutakufa."
15:33 Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema.
15:34 Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!
15:35 Lakini mtu anaweza kuuliza: "Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani wakati watakapokuja tena?"
15:36 Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota.
15:37 Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye.
15:38 Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee.
15:39 Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine.
15:40 Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine.
15:41 Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri.
15:42 Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika.
15:43 Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu.
15:44 Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho.
15:45 Maana Maandiko yasema: "Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;" lakini adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uzima.
15:46 Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida kisha ule mwili wa kiroho.
15:47 Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni.
15:48 Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni.
15:49 Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyohuyo aliyetoka mbinguni.
15:50 Basi, ndugu, nasema hivi: kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki Ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika.
15:51 Sikilizeni, nawaambieni siri: sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa
15:52 wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana mbiu itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa.
15:53 Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa.
15:54 Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: "Kifo kimeangamizwa ushindi umekamilika!"
15:55 "Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?"
15:56 Ukali wa kifo hutokana na dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika Sheria.
15:57 Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
15:58 Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.
16:1 Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia.
16:2 Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja.
16:3 Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu.
16:4 Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.
16:5 Nitakuja kwenu, baada ya kupitia Makedonia--maana nataraji kupitia Makedonia.
16:6 Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda.
16:7 Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu.
16:8 Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste.
16:9 Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi.
16:10 Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi.
16:11 Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu.
16:12 Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.
16:13 Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu.
16:14 Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo.
16:15 Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi ninyi ndugu zangu,
16:16 muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumikia pamoja nao.
16:17 Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu.
16:18 Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii.
16:19 Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priskila pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika Bwana.
16:20 Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu.
16:21 Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe.
16:22 Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANA THA--BWANA, njoo!
16:23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
16:24 Mapendo yangu yawe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.