1:1 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!
1:2 Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
1:3 kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.
1:4 Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
1:5 Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
1:6 Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.
1:7 Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,
1:8 asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
1:9 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
1:10 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
1:11 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
1:12 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.
1:13 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
1:14 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
1:15 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
1:16 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!
1:17 Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
1:18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
1:19 Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
1:20 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
1:21 Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu.
1:22 Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.
1:23 Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.
1:24 Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
1:25 Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
1:26 Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.
1:27 Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.
2:1 Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.
2:2 Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
2:3 Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu,"
2:4 je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
2:5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda.
2:6 Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani?
2:7 Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
2:8 Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa.
2:9 Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.
2:10 Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.
2:11 Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.
2:12 Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.
2:13 Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.
2:14 Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?
2:15 Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.
2:16 Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?
2:17 Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
2:18 Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.
2:19 Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.
2:20 Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa?
2:21 Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.
2:22 Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.
2:23 Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu."
2:24 Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake.
2:25 Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.
2:26 Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.
3:1 Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu. Kama mjuavyo, sisi walimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine.
3:2 Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote.
3:3 Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka.
3:4 Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka.
3:5 Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa.
3:6 Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe.
3:7 Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote--wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini.
3:8 Lakini hakuna mtu aliyeweza kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua.
3:9 Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huohuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
3:10 Maneno ya laana na ya kusifia hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo.
3:11 Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja?
3:12 Ndugu zangu, je, mti wa mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
3:13 Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aonyeshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima.
3:14 Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli.
3:15 Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani.
3:16 Maana popote palipo na wivu na ubinafsi hapo pana fujo na kila aina ya uovu.
3:17 Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki.
3:18 Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.
4:1 Mapigano na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu.
4:2 Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu.
4:3 Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu.
4:4 Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu.
4:5 Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: "Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa."
4:6 Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu."
4:7 Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni.
4:8 Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki!
4:9 Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa.
4:10 Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.
4:11 Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu.
4:12 Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?
4:13 Basi, sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida."
4:14 Ninyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena.
4:15 Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile."
4:16 Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya.
4:17 Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi.
5:1 Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni.
5:2 Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo.
5:3 Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Ninyi mmejilundikia mali katika siku hizi za mwisho!
5:4 Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana, Mwenye Nguvu.
5:5 Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.
5:6 Mmemhukumu na kumwua mtu asiye na hatia, naye hakuwapigeni.
5:7 Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli.
5:8 Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia.
5:9 Ndugu zangu, msinung'unikiane ninyi kwa ninyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia.
5:10 Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana.
5:11 Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema.
5:12 Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni "Ndiyo" kama maana yenu ni ndiyo, na "La" kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu.
5:13 Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa.
5:14 Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.
5:15 Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa.
5:16 Basi, ungamanianeni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi.
5:17 Eliya alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.
5:18 Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake.
5:19 Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha,
5:20 fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.