Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 2 Timothy

1:1 Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uzima tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu,

1:2 nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.

1:3 Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka daima katika sala zangu.

1:4 Nakumbuka machozi yako na ninatamani usiku na mchana kukuona, ili nijazwe furaha.

1:5 Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.

1:6 Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.

1:7 Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.

1:8 Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu.

1:9 Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya matendo yetu wenyewe bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo katika Kristo Yesu kabla mwanzo wa nyakati;

1:10 lakini sasa imefunuliwa kwetu kwa kuja kwake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uzima usio kufa.

1:11 Mungu amenichagua mimi niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema,

1:12 nami nateseka mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye aweza kukilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka Siku ile.

1:13 Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha, na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu.

1:14 Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.

1:15 Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene.

1:16 Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni,

1:17 ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata.

1:18 Bwana amjalie huruma katika Siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.

2:1 Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu.

2:2 Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia.

2:3 Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo yesu.

2:4 Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.

2:5 Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo.

2:6 Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno.

2:7 Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uyaelewe yote.

2:8 Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri.

2:9 Kwa sababu ya kuihubiri Habari Njema mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo,

2:10 na hivyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele.

2:11 Usemi huu ni wa kweli: "Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye.

2:12 Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana.

2:13 Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe."

2:14 Basi, wakumbushe watu wako mambo haya, na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia.

2:15 Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake, na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.

2:16 Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.

2:17 Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.

2:18 Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.

2:19 Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: "Bwana anawafahamu wale walio wake," na "Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu."

2:20 Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine ni vya matumizi ya pekee na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

2:21 Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema.

2:22 Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi.

2:23 Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi.

2:24 Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu,

2:25 ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli.

2:26 Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.

3:1 Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.

3:2 watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;

3:3 watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;

3:4 watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.

3:5 Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.

3:6 Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina;

3:7 wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli.

3:8 Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose.

3:9 Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.

3:10 Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu,

3:11 udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.

3:12 Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.

3:13 Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe.

3:14 Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako.

3:15 Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.

3:16 Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili,

3:17 ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.

4:1 Nakuamuru mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme:

4:2 hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote.

4:3 Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia walimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kusikia.

4:4 Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo.

4:5 Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali; vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema, timiza kikamilifu utumishi wako.

4:6 Kwa upande wangu mimi, niko karibu kabisa kutolewa dhabihu na wakati wa kufariki kwangu umefika.

4:7 Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safari yote na imani nimeitunza.

4:8 Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana Hakimu wa haki, atanipa mimi Siku ile na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake.

4:9 Fanya bidii kuja kwangu karibuni.

4:10 Dema ameupenda ulimwengu huu akaniacha na kwenda zake Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia, na Tito amekwenda Dalmatia.

4:11 Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mpate Marko uje naye, kwa maana ataweza kunisaidia katika kazi yangu.

4:12 Nilimtuma Tukiko kule Efeso.

4:13 Utakapokuja niletee koti langu nililoacha kwa Karpo kule Troa; niletee pia vile vitabu, na hasa vile vilivyotengenezwa kwa ngozi.

4:14 Yule sonara aitwaye Aleksanda amenitendea maovu mengi; Bwana atamlipa kufuatana na hayo matendo yake.

4:15 Jihadhari naye kwa sababu aliupinga ujumbe wetu kwa ukali.

4:16 Wakati nilipojitetea kwa mara ya kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu; wote waliniacha. Mungu asiwahesabie kosa hilo!

4:17 Lakini, Bwana alikaa pamoja nami, akanipa nguvu, hata nikaweza kuutangaza ujumbe wote, watu wa mataifa wausikie; tena nikaokolewa katika hukumu ya kifo kama kinywani mwa simba.

4:18 Bwana ataniokoa na mambo yote maovu, na kunichukua salama mpaka katika Utawala wake wa mbinguni. Kwake uwe utukufu milele na milele! Amina.

4:19 Wasalimu Priska na Akula, pamoja na jamaa ya Onesiforo.

4:20 Erasto alibaki Korintho, naye Trofimo nilimwacha Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa.

4:21 Fanya bidii kuja kabla ya majira ya baridi. Ebulo, Pude, Lino na Klaudia wanakusalimu; vilevile ndugu wengine wote.

4:22 Bwana awe nawe rohoni mwako. Nawatakieni nyote neema.


Next: Titus