Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Titus

1:1 Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu,

1:2 ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uzima wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uzima huo kabla ya mwanzo wa nyakati,

1:3 na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo nuutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu.

1:4 Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu.

1:5 Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu:

1:6 mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi.

1:7 Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo.

1:8 Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu.

1:9 Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho ya kweli na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo.

1:10 Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, wanaowapotosha wengine kwa upumbavu wao.

1:11 Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha.

1:12 Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: "Wakrete, husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!"

1:13 Naye alitoboa ukweli kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu.

1:14 Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli.

1:15 Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa.

1:16 Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.

2:1 Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho safi.

2:2 Waambie wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.

2:3 Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,

2:4 ili wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,

2:5 wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.

2:6 Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi.

2:7 Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako.

2:8 Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.

2:9 Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao,

2:10 au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu.

2:11 Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

2:12 Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa,

2:13 tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

2:14 Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema.

2:15 Basi, fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.

3:1 Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema.

3:2 Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikizano, wawe daima wapole kwa kila mtu.

3:3 Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukawachukia.

3:4 Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu, ulipofunuliwa,

3:5 alituokoa. alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali alituokoa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.

3:6 Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu,

3:7 ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.

3:8 Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu, wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, ambayo ni mambo mazuri na ya manufaa kwa watu.

3:9 Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya Sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu.

3:10 Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye.

3:11 Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.

3:12 Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.

3:13 Jitahidi kumsaidia mwana sheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji.

3:14 Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa.

3:15 Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.


Next: Philemon